Mwanariadha Faith Kipyegon ambaye ameingia katika rekodi za dunia kuwa mwanariadha bora wa mwaka huu katika tuzo zilizofanyika jijini Monaco Ufaransa na kuwa mwanariadha wa kwanza wa kike kutoka hapa nchini kushinda tuzo hilo ameeleza kufurahishwa na matunda ya bidii alofanya mwaka huu katika mashindano mbalimbali.
”Kwa kweli nasikia furaha sana kwa umbali huu. Najivunia kwa kutia juhudi katika mwaka mzima nimepambania kufika hapa. Imekuwa kama ndoto vile.” Alisema Kipyegon baada ya kupewa tuzo lake.
Wakati akizidi kupiga sherehe ya ubingwa hapa nchini katika hotuba ya sikukuu ya Jamhuri, rais William Ruto amempa heshima ya kipekee Faith Kipyegon kwa kumpa utambuzi wa kipekee wa ‘Elder of the Order of the Golden Heart’ (E.G.H.) utambuzi ambao hupewa mkenya ambaye ametendea huduma vilivyo taifa la Kenya na Faith kulingana na Ruto ametunukiwa kwa kuwakilisha au kupeperusha bendera ya Kenya kimataifa.
”Faith Kipyegon ameridhisha sana mwaka huu na anastahili utambuzi huu wa hadhi. Kwa kweli Faith ni mfano mwema wa kuigwa na wanariadha wengine wachanga. Vilevile nawatambua wengine ambao wanajituma katika kuheshimisha taifa hili katika ramani ya dunia. Kongole kwao.” Alisema Ruto
Tuzo hilo hupeanwa na serikali ya wakati huo kama njia moja ya kuenzi wakenya wazalendo na wenye mchango kwa taifa lao.
Vilevile Ruto amesema kwamba analenga kuimarisha zaidi sekta ya michezo pamoja na kutambua mchango mkukubwa unaoletwa na wanariadha pamoja na wachezaji wengine kwa Kenya kutokana na juhudi zao viwanjani.

