RAIS RUTO ASEMA KENYA IMEPIGA HATUA KIMICHEZO

Rais William Samoei Ruto anasema kwamba Kenya imepiga hatua katika michezo baada ya miradi kadhaa kuzinduliwa ikiwemo Talanta Hela uliozinduliwa rasmi mwezi Juni mwaka huu.

Akihotubia taifa jana katika sherehe za siku kuu ya Jamhuri  jijini Nairobi  Ruto alisema kuwa  wachezaji wa Kenya wanazidi kuipa sifa nchi hii kupitia juhudi zao viwanjani katika mashindano ya kimataifa na kuwapongeza kwa kuonyesha uzalendo.

Aliwapongeza akina Ferdinand Omanyala ambaye ni mtimkaji mwenye kasi zaidi barani Afrika kwa kasi ya 9.77, kwa kuonyesha ukakamavu wao kuwakilisha taifa, timu ya taifa ya raga Kenya Shujaa lakini pia wanariadha waliofuzu kwa mashindano ya olimpiki yanayotarajiwa kufanyika jijini Paris Ufaransa mwaka 2024.

Hata hivyo Ruto jana aliwapa utambuzi wa kipekee wanariadha mbalimbali akiwemo Faith Kipyegon, heshima ya EGH, utambuzi ambao serikali huwapa wananchi wake kwa kudumisha uzalendo pamoja na kuwakilisha taifa ya Kenya kimataifa.