Wajumbe saba wa timu ya matibabu waliomtibu mchezaji maarufu wa soka kutoka Argentina, Diego Maradona, kabla ya kifo chake, wamefunguliwa mashtaka hii leo kwa tuhuma za mauaji yasiyo ya kukusudia.
Diego Maradona alifariki dunia kutokana na shambulio la moyo mwaka 2020, akiwa na umri wa miaka 60, huku akitoka katika upasuaji wa ubongo na akiwa katika hatua ya kupona.
Mwaka mmoja baada ya kifo chake, waendesha mashtaka wamesema uchunguzi wao umeonesha kwamba kifo chake kingeweza kuepukika, wakilalamikia kulikuwa na uzembe wa kimatibabu.
Timu ya watabibu wa Maradona imekana mashtaka hayo, ikidai kuwa ni Maradona mwenyewe aliyesusia matibabu na kwamba alipaswa kubaki hospitalini kwa muda zaidi baada ya tiba ya upasuaji aliyokuwa amefanyiwa.
Walio na msimamo kwamba alipaswa kupewa uangalizi wa hali ya juu zaidi kimatibabu wamepania kesi hiyo wakisema wanataka kuona haki ikitindeka.
Hata hivyo maoni ya wengine ni kuwa kifo hicho ilikuwa kazi ya Mungu ambayo haina makosa.
Mahakama katika mji wa San Isidro, mjini Buenos Aires, itasikiliza ushahidi wa karibu mashahidi 120 na inaweza kudumu hadi zaidi ya mwezi.
Ni kesi inatazamiwa kuzua msisimko mkubwa nchini Argentina, ambapo Maradona anashabikiwa mno/
Baadhi ya sifa kuu za Maradona ni jinsi alivyosaidia pakubwa katika ushindi wa taifa lake la Argentina na Kombe la Dunia mwaka 1986, hivyo kupewa heshima ya shujaa wa kitaifa.
Kipaji chake kama mchezaji hodari na machachari kilimzolea umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi lakini alitumbukia katika changamoto kubwa za kibinafsi katika maisha yake- mfano ukiwa uraibu wa pombe na dawa za kulevya