Inspekta jenerali wa polisi Douglas Kanja, amekashifu vikali hatua ya mkenya anayefahamika kama Collins Chepkulei, kufungua kituo cha polisi katika eneo la Cherus kaunti ya Uasin Gishu.
Kulingana na Kanja, hatua hiyo ni makosa makubwa kwani raia huyo, alikosa kufuata sheria na utaratibu hitajika, ili kutekeleza suala hilo licha yake kuwa na manufaa kwa wananchi.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa, inspekta mkuu wa polisi amesema kuwa wananchi wa eneo hilo, walipaswa kuwasilisha malalamishi yao kwa afisi za viongozi wao kwenye serikali, pamoja na kamishna wa eneo bunge hilo.
Kanja amesema kuwa idara ya usalama, ndiyo iliyo na jukumu la kisheria kufungua kituo cha polisi.
Vile vile Kanja amewataka maafisa wa polisi kutosheka na mishahara yao na kujitenga na masuala ya ufisadi.
Aidha amesema kuwa hatua ya maafisa wa polisi kuitisha hongo, ni ishara ya utovu wa nidhamu kazini na kinyume cha sheria na maafisa wa polisi wanapaswa kuendeleza majukumu yao kwa uadilifu na kujitolea.
Kwa upande wake naibu inspekta jenerali wa polisi Eliud Lagata, ameahidi kuongoza maafisa wa polisi katika kukabiliana na ulangazi, pamoja na utumizi wa mihadarati nchini.