Mkufunzi wa klabu ya Malindi Progressive Elly Katana ametilia pondo suala la kuwepo kwa ushirikinna viwanjani hasa katika soka la kaunti ya Kilifi.
Mkufunzi huyo ambaye klabu yake ilipoteza katika mechi ya ‘Mudzini dabi’ kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Young Bulls katika uwanja wa Alaskan amethibitisha ukweli wa kauli za baadhi ya mashabiki kwamba kuna baadhi ya vilabu mashinani vinatumia mazingaombwe ili kupata mafanikio viwanjani.
“Ile kitu mashabiki wanasema ni ukweli kabisa, kwa kweli kuna ushirikina mwingi sana. Lakini ushirikina hausaidii kitu. Mazoezi na bidii ndio huleta matokeo. Ingekuwa uchawi unasaidia saa hii Nigeria au hata Tanzania wangekuwa wameshinda kombe la dunia.”
Mkufunzi huyo ameshauri wachezaji pamoja na baadhi ya wakuu wa vilabu kujiepusha na masuala hayo ya ushirikina akihoji kwamba vilabu kama hivyo kufifia na kupotea kabisa punde tu baada ya nguvu za dawa hizo za giza kuisha makali yake.

