VILABU VYA MASHINANI VYAPEANA ‘WALK OVER’ SANA KISA UKOSEFU WA HELA

Klabu ya Deep Sea kutoka kaunti ya Lamu jana ilizawadiwa alama tatu na mabao 2-0 kutokana na wapinzani wao Inter Dabaso kutoka mji wa watatu kaunti ya kilifi kukosa kuheshimu ratiba.

Hii inakuwa ni mechi ya tano katika kipindi cha mwezi mmoja kwenye ligi ya daraja la pili kitaifa vilabu vinakosa kuhesimu ratiba katika mechi za ugenini.

Hivi majuzi klabu ya Maji Bombers kutoka Lango Baya kaunti ya Kilifi ilipewa adhabu ya kutolewa kwenye ligi hiyo kutokana na kukosa kuheshimu ratiba za mechi, hali hiyo ikitajwa kuwa imechangiwa kwa vilabu vingi mashinani  kukumbwa na ukata wa kifedha jambo ambalo linapelekea vilabu hivyo kukosa kumudu gharama ya juu ya kusimamia mechi.

Klabu ya Yanga FC inayoongozwa na mkufunzi Collins Omol ilisajili sare ya mabao 2-2 katika dimba la ugenini dhidi ya Simba Apparel katika uwanja wa Changamwe Estate.

Katika dimba lingine ni kwamba Kishada walipoteza nyumbani kwao dhidi ya Omax FC  ya mkufunzi Juma Kalato kwa kichapo cha mabao 4-1.

Mechi kati ya Samburu Lions na klabu ya Beach Bay ililazimika kusitishwa katikati ikiwa sare ya bao 1-1 kutokana na vurugu iliyotokea uwanjani iliyotokana na Beach Bay kulalamikia maamuzi mabaya ya refa katika mechi hiyo.