SHOKA LAITOA JUVENTUS KUTOKA NAFASI YA UEFA HADI ‘MTAA WA SABA’

Klabu ya Juventus, Italia imepigwa shoka la alama kumi baada ya maamuzi mapya ya mahakama ya shirikisho la soka la Italia iliyoafiki ukweli wa uchunguzi kwamba miamba hao wa Serie A walihusika katika udanganyifu katika masuala ya mahesabu ya fedha kipindi cha uhamisho.

Kutolewa kwa alama kumi kwa Juventus sasa kunaifanya klabu hiyo kukosa matumaini ya kumaliza katika nne bora ili angalau kushiriki mashindano ya Uefa msimu ujao kwani sasa wameshuka hadi nafasi ya saba.

Ikumbukwe kwamba klabu hiyo ilikuwa imepigwa pigo la kupunguziwa alama 15 mapema mwaka huu kutokana na udanganyifu ila uamuzi huo kubatilishwa mwezi uliopita.

Baadhi ya viongozi wa soka katika klabu hiyo akiwemo Andrea Agnelli ambaye ni rais wa zamani wa klabu hiyo wamepigwa marufuku ya kutojihusisha na soka kutokana na uamuzi huo mpya.