SANGO SPORTIFF YAZIDI KUANDIKISHA MATOKEO MAZURI KWENYE MSIMU WAO WA KWANZA DARAJA LA PILI

Mkufunzi wa klabu ya Sango Sportiff Righo Jillo amesema kwamba ana matumaini makubwa kuwa klabu hiyo inayoshiriki ligi ya daraja la pili kitaifa itazidi kuandikisha matokeo mazuri na hatimaye kupanda hadi daraja la kwanza mwisho wa msimu.

Ameyasema hayo baada ya wikendi ilopita kusajili ushindi wa kishujaa dhidi ya klabu ya Beach Bay kutoka magarini walipoitandika kichapo cha mabao 5-2 katika dimba lao la Santiago, uwanja ulioko eneo bunge la Garsen kaunti ya Tana River.

Mkufunzi Jillo amesema kwamba klabu hiyo inapata motisha kutoka kwa nguvu ya mashabiki wa timu hiyo ambayo amekiri kuwa wamekuwa na mchango mkubwa katika kuifanya klabu hiyo kusimama msimu huu.

Sango inashiriki ligi ya daraja la pili kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kuandikisha matokeo mazuri katika ligi ya mkoa msimu uliopita. Klabu hii yenye makazi yake katika mtaa wa Sailoni, ndio klabu pekee inayoshiriki ligi kubwa katika kaunti hiyo ya Tana River.