Mkufunzi wa klabu ya Furunzi FC Nero Chishenga sasa amethibitisha kwa maneno yake mwenyewe kwamba ameachana na klabu hiyo inayocheza daraja la pili kitaifa.
Kocha Nero mwenye umri wa miaka 30 ameachana na klabu hiyo baada ya kuingoza klabu hiyo kutoka ligi ya mkoa hadi daraja la pili kitaifa.
”Mimi sina shida na wachezaji, wale wapo vizuri tu. Lakini mimi kutokana na masuala ya uongozi nimeamua kuachana na klabu hiyo. Kuna baadhi ya mechi sijakuwa uwanjani, nlikuwa naboycott tu lakini nilikuwa nishajitoa kitambo. Nataka kuisema rasmi saa hii napania kujihusisha na mambo mengine na klabu nyingine”
Amewashauri wachezaji wake kuwa makini kutotilia maanani uchochezi kutoka kwa viongozi wengine wenye nia ya kuvunja vilabu na badala yake kuzingatia mazoezi yatakayokuza vipaji vyao.
Mkufunzi Nero amekuwa akisusia kujitokeza kwenye mechi kama mkufunzi mkuu wa klabu hiyo kutokana na mgongano ulioko katika klabu yake.
Mgogoro huo umekuwa ukisababisha kudorora kwa matokeo katika klabu hiyo msimu huu ambao ndio wao wa kwanza katika daraja la pili.
Moja ya mafanikio ya mkufunzi Nero Chishenga katika klabu ya Furunzi ni kuishindia klabu hiyo kombe la Talanta soka mwaka jana.

