Huenda michezo katika eneo bunge la Magarini ikaimarika hata zaidi baada ya mbunge wa eneo hilo Harry Kombe kufanya kikao hii leo na wadau wa michezo mbalimbali katika eneo hilo kujadili masuala ya michezo ambayo yanahusu vilabu vya mashinani.
Harry Kombe ameahidi kusaidia wachezaji na mabasi ya usafiri katika mechi za mbali na karibu ili kuona kwamba vilabu vinaheshimu ratiba pamoja na kuwanunulia wachezaji sare za soka pamoja na kulipia vilabu nusu ya hela za kujiandikisha na kushiriki ligi mbalimbali.
Kombe hii leo katika eneo la gongoni ameanzisha mchakato wa kufufua Timu ya Mkombozi ambayo ilikuwepo miaka ya zamani. Mbali na soka ameaahidi wanamichezo wa eneo bunge hilo atatengeneza timu za kila mchezo itakayowakilisha eneo bunge hilo.
Kwa upande wake mwenyekiti wa FKF tawi la eneo bunge hilo Julius Mweni amempongeza Harry Kombe kwa kuchukua hatua hiyo huku akithibitisha kwamba eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi ndio eneo pekee Kenya nzima ambalo vilabu vinavyoshiriki ligi yake havilipishwi ada ya kushiriki kwenye ligi.

