OMAX FC NDIO MABINGWA WA LIGI YA DARAJA LA PILI

Klabu ya Omax FC Kutoka Mombasa inayoongozwa na mkufunzi Juma Kalato ndio mabingwa wa ligi ya daraja la pili kitaifa baada ya wikendi hii kusajili ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya nafasi ya pili Simba Apparel.

Kufuatia ushindi huo wa alama tatu sasa Omax imeweka pengo la alama 11 na moja kwa moja kutangazwa mabingwa kutokana na kuwa sasa kumesalia mechi tatu msimu wao kutamatika.

Matokeo mengine katika daraja la pili ni kuwa Beach bay walipiga sare tasa dhidi ya Ashton Rangers katika uwanja wa Mjanaheri ulioko Gogoni eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi. Samburu Lions kutoka kwale ilipiga sare tasa pia dhidi ya klabu ya Tana River Sango Sportiff inayoongozwa na mkufunzi Righo Jillo.

Licha ya klabu yaYoung Bulls wikendi hii kusajili ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Dandora Youth, bado watasalia katika nafasi ya pili baada ya vinara wa sasa wa Ligi hiyo Rainbow fc pia kusajili ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wenyeji wao Liberty Sports Academy.

Kwa sasa Rainbow inaongoza ligi hiyo na alama 65 ikiwa imeishinda Young Bulls kwa utofauti wa mabao. Kibra united nayo ilicheza mechi wikendi hii na walitandikwa nyumbani kwao kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Nairobi United ambao sasa wamekwea hadi nafasi ya tatu na alama 62.