Klabu ya Mariakani Fc kutoka kaunti ya Kilifi inayoshiriki ligi ya daraja la pili kitaifa inalilia udhamini kwani sasa inapitia kipindi kigumu kiuchumi wakati huu ambapo ligi imeingia katika raundi ya pili.
Hayo yanajiri baada ya wikendi ilopita mechi yao kusitishwa baada ya kipindi cha kwanza pale ambapo klabu hiyo ilishindwa kulipa hata hela ya refa wa katikati ya uwanja jambo ambalo lilisababisha mechi hiyo kupigwa breki.
Kabla ya kusimamishwa, mechi hiyo dhidi ya klabu ya Beach Bay ilikuwa vibaya upande wao kwani tayari wageni Beach Bay wanaoongozwa na kocha James Mkutano walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kwa sasa Mariakani Fc inasimama katika eneo hatari la kushuka daraja kwani ni ya mwisho katika jedwali la ligi hiyo wakiwa na alama 20 pekee baada ya mechi 25.
Msimu ukianza klabu hiyo (Mariakani Fc ) walianza vizuri wakiwa kati ya miamba ambao wangekuwa wanapigania nafasi ya kupanda daraja hadi Div One msimu ujao.
Kwa sasa klabu ya Bumbani Stars inasimama katika nafasi ya kwanza ligini, na vijana hao wa kocha Bakari wako na alama 61 baada ya kupewa alama tatu wikendi ilopita baada ya Ashton Rangerskukosa kuheshimu ratiba kutokana na ukata wa kifedha.

