MASHABIKI WA KENYA WAOMBA UDHAMINI

Mashabiki wa timu ya taifa ya soka hapa nchini Harambe Stars kupitia chama chao KEFOFA wanalilia ufadhili wa usafiri kutoka kwa serikali kuu, Shirikisho la Soka Kenya FKF na wahisani wakitaka ufadhili kusafiri kwenda kuisapoti Harambee Stars katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 nchini Malawi mwezi ujao.

Timu ya taifa Harambee Stars itakuwa inavaana na Burundi tarehe 7 mwezi Juni na kisha ivaane na mabingwa wa Afrika Cote d’Ivoire tarehe 11 katika mechi za Kundi E.

Harambee Stars inayoongozwa na kocha Engin Firat itacheza mechi zake za nyumbani ugenini kwa sababu viwanja vya nyumbani  Nyayo na Kasarani vinakarabatiwa kwa sasa na hakuna uwanja mwengine wenye hadhi ya mechi hizo hapa nchini.

Uwanja wa Kasarani unatarajiwa kuwa  mwenyeji wa Kombe la AFCON  2027, huku Nyayo ikiandaa kipute cha CHAN baadaye mwaka huu.