‘MANUSURA’ WAUNDA TIMU YA SOKA DABASO

Vijana wa Dabaso katika eneo la watamu Kaunti ya kilifi  ambao walikuwa wameathirika na dawa za kulevya  sasa wameunda timu ya soka ili kujishuhulisha viwanjani na kutumia wakati wao mwingi kuboresha afya zao pamoja na talanta zao ili kuepuka majaribu ya kurejea katika tabia zao za awali.

Melda Mnyazi ambaye ni afisa wa michezo katika kaunti ya kilifi anasema wamelazimika kuunda timu hiyo majuma kadhaa yaliyopita ili kuitikia wito wa wakazi wa Dabaso kuwakomboa vijana wao kutoka jinamizi la mihadarati.

”Tumeunda hii himu kutokana na shinikizo la wakazi au jamii ya Dabaso Watamu kuhusu kuwaepusha vijana hawa kutokana na matumizi ya dawa za kulevya. Hapo ndio tukaja pamoja na kuizalisha timu hii ambayo kwa sasa hatujaipatia jina rasmi lakini tunaiita Recoverees japo jina rasmi litakuja karibuni.” Alisema Melda.

Mnyazi anasema kwamba wanashirikiana na serikali ya kaunti ya kilifi kuwafanya vijana hao kuzindua talanta pamoja na kufanya talanta zao kuwa ajira mbali na burudani la michezo pekee.

”Tumekuja pamoja na serikali ya kaunti pamoja na uongozi wa michezo kilifi kusaidia hawa vijana wapate kipato kupitia talanta. Hawa vijana wanahitaji kitu cha kufanya baada ya kujiondoa michezoni wasije wakarejea huko tena.” Aliongeza Melda.