LETENI MICHEZO LAMU, TUACHE UHALIFU

Vijana wa eneo la Witu katika kaunti ya Lamu wametoa wito kwa viongozi wa serikali kuwahusisha kwenye michezo ili vijana hawa wasijihusishe na magenge ya uhalifu.

Uwepo wa changamoto za kiusalama katika wadi ya witu ndio jambo lililopelekea Suleiman Farah ambaye ni mwakilishi wadi wa eneo hilo kuanzisha mashindano ya soka ambayo yamehusisha vilabu zaidi ya ishirini.

Kulingana na Farah ni kwamba mashindano hayo yanalenga kuleta pamoja jamii ambazo zimekuwa zikizozania ardhi baina ya wafugaji na wakulima pamoja na vijana ambao hujihusisha na mashambulizi ya kikaidi.

Ni kauli ambayo imeungwa mkono na Ismael Barisa ambaye ni mwanaharakati wa masuala ya vijana aliyesema kwamba ujio wa mashindano hayo ni kati ya mbinu zitakazosaidia kuhamasisha jamii kuhusu suala zima la amani pamoja katika kaunti nzima ya Lamu.