Huenda wachezaji wa klabu ya Gor Mahia wakapata makazi rasmi katika siku za usoni kama njia moja ya kuzidi kuimarisha miundo msingi ya klabu hiyo kulingana na hadhi yake kitaifa na kimataifa.
Hiyo ni kulingana na Eliud Owalo ambaye ni waziri wa masuala ya teknolojia na mawasiliano nchini lakini pia shabiki sugu wa klabu hiyo.
Amethitibisha kuwa basi alilowatunuku Kogalo mwanzoni mwa msimu limechangia pakubwa urahisishwaji wa safari zao na kuwafanya kutetea ubingwa wao msimu huu pamoja na kujishindia kombe lao la FKF kwa mara 21.
”Kwa kuwa klabu hii imeonyesha uwezo mkubwa, tutaanza mipango ya kuitafutia klabu hii na wachezaji makao rasmi na kuijengea uwanja wao ili kuwawezesha kuzidi kufanya bora viwanjani. Hii timu sasa inataka kuanza upesi matayarisho ya mashindano ya kimataifa ya CAF ili kuona kwamba tunaanza kusajili makombe ya kimataifa kwani uwezo klabu hii uko nao” Alisema Owalo.

