Mchezaji wa timu ya taifa ya Junior Starlets Marion Serenge amethibitisha kuwa analenga kushiriki mashindano ya kombe la dunia 2024 kwa wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 katika Jamhuri ya Dominika mwishoni mwa mwaka huu.
Hii ni baada ya taarifa kuwa huenda mashindano hayo yakakinzana na wakati wa mitihani ya kitaifa ya KCSE.
Marion amesema yupo tayari kuachana na mtihani na badala yake kushiriki kombe la dunia baada ya kufanya mashauriano na baba yake mzazi.
Fred Serenge ambaye ni mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Kenya amethibitisha kuwa atamruhusu mwanawe kucheza badala ya kufanya mitihani mwaka huu akihoji kuwa mtihani wa KCSE kufanyika kila mwaka huku World Cup. Ikifanyika baada ya miaka minne.
Hata hivyo ameshauri serikali ya Kenya kuahirisha mitihani ya wanafunzi hao ambao ni wachezaji na kuwatengea muda wa kuifanya baada ya kuhudumia taifa michezoni.
Timu ya Junior Starlets ilifuzu kwa Mashindano ya kimataifa ya kombe la dunia na ndio timu pekee kutoka Kenya kwenye soka kuwahi kushiriki katika kipute hicho.

