VIONGOZI WA WIPER MOMBASA WAMKOSOA RAILA 

Viongozi wa chama cha Wiper tawi la Mombasa wamejitokeza na kukosoa vikali hatua ya kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga ya kuingia kwenye mazungumzo na serikali.

Viongozi hao wanadia kwamba kitendo hicho cha Raila kinahujumu makubaliano ya muungano huo wa Azimio huku wakiongeza kuwa mazungumzo hayo ni kwa faida ya Raila pekee na chama cha ODM.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa Wiper tawi la Mombasa Francis Mulinge, viongozi hao wamemshinikiza kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka kudinda kujiunga katika mazungumzo hayo baada ya kudhalilishwa.

“Raila tunamjua hana msimamo, na pia tunajua anataka kuvunja muungano wa Azimio na hatuwezi kubali Azimio ivunjike.” Amesema Mulinge.

Vile vile wamekashifu kitenzo cha wahuni kuvuruga hotuba ya Kalonzo Musyoka siku ya Jumatano wakidai hiyo ni njama fiche ya kutaka kumzima kisiasa kiongozi huyo wa Wiper, hatua wanayosema inaashiria mtikisiko katika muungao wa Azimio.

Kwa sasa viongozi hao wamemuomba Kalonzo kuchukua muda huu na kuanza kutafuta uungwaji mkono wa mapema katika kinyang’anyiro cha urai cha mwaka 2027.

“Kalonzo anafaa apewe heshima maana amemshikilia Raila kwa muda mrefu bila shukrani yoyote. Kwa sasa Kalonzo tunakuomba uachane na Raila na sisi tutakuunga mkono usimame kiti cha urais uchaguzi ujao.” Charles Mutisya, kiongozi wa vijana Wiper Mombasa.