Shuhuli za michezo katika kaunti ya Tana River na sehemu tofauti za pwani zimepata pigo kutokana na mvua nyingi inayoendelea kunyesha.
Katika kaunti ya Tana River kwa mfano huenda ligi ya soka kaunti ya Tana River ikasitishwa kwa muda katika baadhi ya maeneo kufuatia mafuriko ambayo yanaendelea kukumba kaunti hii na kuathiri maelfu ya wakazi pamoja na wachezaji.
Mwenyekiti wa FKF Said Ilu, anasema tayari wamesitisha shughuli za soka eneo la Mororo kufuatia mafuriko huku pia wakiendelea kutathmini hali katika upande wa Makere kwani pia sehemu hii imeanza kufurika.
Katika kaunti ya Kilifi, Klabu ya Gabba FC ikiongozwa na mkufunzi Davis Chadi inalilia wahisani pamoja na viongozi wa serikali kuingilia kati kwani vilabu vimepata pigo kiuchumi.
”Tunaomba wahisani waje huku mashinani hasa kwa hizi timu zetu za Zone C, waje wawasaidie wachezaji. Tunategemea mimea mashambani lakini kwa sasa imebebwa na mafuriko. Mimea hiyo tungeuza tukapata hela za refa na matumizi mengine sasa tunaumia” Alisikitika Chadi

