Mkufunzi mkuu wa timu ya taifa ya Harambee Stars Engin Firat ana mashaka kuwa Kenya itakuwa tayari kuandaa mechi zijazo za kufuzu kwa Kombe la Dunia hapa nyumbani mwezi Juni, dhidi ya Burundi na mabingwa wa Afrika Ivory Coast.
Kocha huyo akizungumza masaa machache kablaya Harambee Stars kuanza safari yao ya Malawi anasema kukosekana kwa viwanja vilivyoidhinishwa na FIFA kunaweza kuhatarisha kampeni ya Stars katika kujaribu kufuzu kwa fainali kubwa zaidi ya kandanda 2026.
Kwa sasa, Kasarani imefungwa kwa maboresho kwa maandalizi ya AFCON 2027, huku uwanja mwingine pekee mbadala wa Nyayo haujafanyiwa ukarabati ili kufikia viwango vya FIFA kwa mechi za kitengo A.
Wakati huo huo, Firat amefichua kukosekana kwa wachezaji wa kawaida katika kikosi chake kunaweza kumlazimisha kutumia mtindo mpya katika mechi za kirafiki za wikendi hii nchini Malawi, dhidi ya Zambia, Zimbabwe na wenyeji.

