CHADI ALALAMIKIA HELA YA UHAMISHO FKF

Mkufunzi wa klabu ya Gabba United Joshua Chadi wa klabu inayoshiriki ligi ya kaunti ya Kilifi kwa sasa amepinga sheria mpya iliyopendekezwa ya ada ya uhamisho wa wachezaji katika ligi ya eneo bunge la Malindi.

Kulingana na Chadi ada ya shilingi 3000 ambayo ilipendekezwa ni kubwa mno na haifai kuwa kwani tayari kwa sasa vilabu vya mashinani vinapitia changamoto za kupata angalau fedha za kujisajili kwa ligi msimu mpya ukitarajiwa kuanza majuma mawili yajayo.

Amesema ada  hiyo huenda ikalemaza ukuaji wa talanta za wachezaji mashinani kwani itafungia wachezaji kupata fursa za ngazi za juu kuonyesha talanta zao.

Amethibitisha kuwa ili kuinua talanta za wachezaji binafsi ni sharti viongozi waje pamoja na kujadili kwa ukubwa jinsi ya kugeuza au kuandaa mfumo tofauti. Amekiri kuwa sio sahihi kufungiwa kwa mchezaji kisa shilingi elfu tatu za uhamisho kwani hiyo kimtazamo wake huenda ikasambaratisha vipaji vya Malindi.