Kusambaratika kwa klabu ya Maji Bombers iliyokuwa inashiriki katika ligi ya fkf daraja la pili ya kitaifa kumechangia pakubwa kudororora kwa viwango vya soka katika wadi ya Jilore eneo bunge la Malindi kaunti ya Kilifi.
Akizungumza na Tama la Spoti kupitia njia ya simu mkufunzi anayeshikilia klabu hiyo kwa sasa Max Khonde amethibitisha kuwa timu ya Maji Bombers ilikuwa imesheheni wachezaji kutoka maeneo mengi jambo ambalo linatamausha vijana wengi na wapenzi wa soka kutoka eneo hilo.
Khonde ameomba viongozi wa wadi ya Jilore lakini pia eneo bunge la Malindi pamoja na washikadau mbalimbali kuja pamoja na kushirikiana kuifufua klabu hiyo kwani sasa hawana Tumaini la kushiriki ligi yoyote kutokana na ukata wa kifedha.
Maji Bombers walishushwa daraja msimu uliopita kutokana na kukosa kuheshimu ratiba za mechi katika kaunti ya Lamu na Taita Taveta kutokana na ukata wa kifedha baada ya basi walilokuwa wakitumia la kampuni ya Coast Water pia nalo kuharibika.

