BAK YAJIANDAA KWA KYISA MWEZI APRILI

Kaunti ya kilifi inazidi kujiimarisha kwa ajili ya kuwa wenyeji wa mashindano ya kitaifa ya KYISA yatakayofanyika mwezi Aprili mwaka huu. Kati ya michezo itakayojumuishwa katika mashindano hayo ni soka, voliboli lakini pia mpira wa vikapu.

Kulingana na mkufunzi Frank Osogo ambaye anasimamia mpira wa vikapu katika kaunti ya Kilifi ni kuwa wanalenga kufanya majaribio ya wachezaji kuanzia 23 mwezi huu katika kiwanja kipya cha Cleopatra Malindi kisha kufanya majaribio tena Kilifi katika chuo kikuu cha Pwani tarehe 24.

Wachezaji wa kike na kiume wenye umri kati ya miaka 18 hadi 23 ndio wanaotafutwa kujiunga na kikosi cha kaunti, na Osogo ameomba vijana wengi kujitokeza kwa ajili ya zoezi hilo.

Osogo amethibitisha kuwa viwanja vitatu katika mji wa Malindi vipo tayari kwa ajili ya kuandaa mashindano hayo ukiwepo uwanja mpya wa Cleopatra, Uwanja wa shule ya upili wa Barani lakini pia ule wa Town Secondary ambako fainali za mashindano hayo zitaandaliwa.