Mwakilishi wadi wa Mnarani Juma Chengo anasema analenga kuanzisha mpango wa kuwahifadhi wachezaji wa timu ya kinadada ya soka mahali pamoja kwa lengo la kuwaandaa wanaposubiri fainali za kombe la Governors Cup zitakazofanyika mwaka huu.
Hii ni baada ya Mnarani Ladies kuibuka mabingwa wa kombe la eneo bunge la Kilifi Kaskazini baada ya kuizidi Matsangoni Ladies kwenye ujuzi wa upigaji wa matuta kwa penalty 4-2 baada ya mechi hiyo kuisha sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida.
Juma Chengo anasema pia analenga kuwasilisha hoja kwa waandaaji wa mashindano ya Governors kuona kwamba fainali zinafanyika katika kipindi cha likizo ya mwezi Aprili ambapo hata wachezaji ambao ni wanafunzi wanaweza kushiriki.
Taarifa zinasema kwamba fainali za Governors Cup, mashindano yanayodhaminiwa na Gavana Gideion Maitha Mungaro zitafanyika kabla mashindano ya Kenya Youth Inter County Sports Association mwezi Aprili.
Kulingana na waandalizi mashindano ya Governors Cup yanatumika kwenye kuchagua kikosi kitakachowakilisha kaunti ya kilifi kwenye mashindano hayo ya kitaifa, historia ikiandikishwa mwaka huu kaunti ya Kilifi ikiandaa mashindano ya KYISA kwa mara ya kwanza kabisa tangia ugatuzi.

