Mwenyekiti wa soka la fkf katika tawi la eneo bunge la Malindi kaunti ya Kilifi Tom Lango amekiri kuwa msimu uliopita kulishuhudiwa ‘ufisadi’ mkubwa wa mabao katika ligi hiyo.
Amesema ufisadi huo ulitokana na tamaa ya zawadi walizokuwa wametangaza watatuza wachezaji mwisho wa msimu kama vile mfungaji bora na kipa bora pamoja na tuzo nyingine.
Amekiri kuwa baadhi ya wachezaji walihonga marefa ili waandikiwe mabao mengi tofauti na matokeo yao uwanjani.
Hata hivyo Lango amesema kuwa msimu huu wanalenga kuimarisha zaidi ligi kwa kuweka mikakati ya kupunguza au hata kumaliza ufisadi huo.
Amethibitisha kuwa msimu uliopita walilazimika kuwafungia marefa wafisadi pamoja na kuwapunguzia mabao wachezaji waliokuwa wameongezewa mabao haramu.
Kwa sasa vilabu mjini Malindi vinajiandaa kwa msimu mpya 2024/2025 utakao anza mwisho wa mwezi huu huku kukiwa na kadirio la vilabu takriban 30 vitakavyoshiriki.

