Mkufunzi mkuu wa timu ya taifa ya Cameroon Rigobert Song amethibitisha kuwa ilikuwa vigumu kwa Andre Onana kucheza kwenye mechi ya AFCON dhidi ya Guinea jana mechi yao ya kwanza katika mashindano hayo.
Ameeleza kipa huyo wa Manchester United aliwasili kambini Ivory Coast kama alichelewa. Yote ikitokana na safari yake ya ndege kuwa na changamoto pale ambapo safari ilikatishwa ghafla maili 150 mbali na jiji la Abijan kutokana na hali ya anga ambapo kulikuwa na ukungu uliofanya marubani kushindwa kuendelea na safari.
Taarifa zasema kwamba Onana alilazimika kusafiri kwa gari barabarani mwendo wa masaa matatu hadi manne jambo ambalo lilimfanya kuwasili saa moja kabla mechi hiyo kuanza.
Tetesi zasema kwamba Onana alizua vurumai baada ya kufahamu hayuko kikosini na ilichukua mchezaji mkongwe Al Hadj Diouf kumtuliza. Onana alikuwa acheze mechi mbili ndani ya masaa 24 baada ya kucheza mechi ya Manchester dhidi ya Tottenham Hotspers iliyoisha kwa mabao 2-2 siku ya jumapili na kisha acheze jana Afcon.
Cameroon jana walipiga sare ya bao 1-1 dhidi ya Guinea (konakry.)
Mkufunzi wa timu ya taifa ya Mali Eric Chelle anaimani kuwa vijana wake watasajili ushindi dhidi ya timu ya taifa ya Afrika Kusini.
Chelle hata hivyo amekiri kuwa Bafana Bafana sio ya kubeza akidokeza kuwa tukio la kuwa wachezaji wengi wa taifa hilo hucheza ligi za nyumbani sio udhaifu hata kidogo kwa hivyo anakwenda katika mechi hiyo akiwa amejitayarisha vilivyo.
Mali watashuka dimbani dhidi ya Afrika Kusini mwendo wa saa tano usiku. Mechi nyingine ya leo ni ile ya Tunisia dhidi ya Namibia. Kwa sasa Burkinafaso wanacheza dhidi ya Mauritania.
Kwa sasa mashindano ya Afcon huko Ivory Coast bado yapo katika hatua ya makundi.

