Mkufunzi wa zamani wa klabu ya Pwani Fc Emmanuel Kazungu ambaye sasa ni katibu mkuu wa fkf katika eneo bunge la Magarini amependekeza viongozi wa eneo hilo kupiga jeki vilabu ambavyo viko katika ngazi za juu kisoka kuzidi kuwakilisha eneo Magarini kuliko kuunda timu mpya ambazo hazijasajiliwa katika ligi yoyote.
Akizungumza na Tama la Spoti jioni ya leo mkufunzi Kazungu amemshauri mbunge wa zamani wa Magarini Harry Kombe kuisaidia Beach bay ambayo inacheza ligi ya daraja la pili tayari kuliko kufufua timu yake ya Mkombozi fc ambayo itakuwa haishiriki ligi yoyote ya FKF.
Hayo yanajiri baada ya Harry Kombe majuma kadhaa yaliyopita kutangaza kwamba analenga kuifufua timu ya Mkombozi Fc na kuanza kutafuta talanta za wachezaji kutoka mashinani mwa eneo hilo, timu ambayo itakuwa inawapa nafasi vijana kupata fursa ya kuonekana katika ngazi za juu viwanjani.
