Klabu ya Gor Mahia ndio mabingwa wa ligi kuu ya fkf hapa nchini Kenya baada ya jana katika mtanangwe wa mwisho kusajili ushindim wa mabao 4-1 dhidi ya klabu ya Nairobi City Stars katika uwanja wa Moi Kasarani, jijini Nairobi.
Kogalo walinyakua ubingwa wao wa 20 kwa utofauti wa alama moja dhidi ya Tusker ya Robert Matano ambao ndio mabingwa watetezi wa ligi hiyo waliosajili ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya klabu ya Vihiga Bullets na kufikisha alama 69 huku Gor Mahia wakimaliza ligi na alama 70.
Licha ya ubingwa huo Gor Mahia wameenda nyumbani na kombe pekee kutoka kwa fkf baada ya kusakata soka kwa msimu mzima. Hii ni baada ya shirikisho la soka linaloongozwa na rais Nick Mwendwa kutangaza kwamba hakuna mgao wa pesa za kupewa bingwa kutokana na msimu kuchezwa bila mdhamini.
Wakati hayo yakijiri, Willis Ojwang ambaye ni meneja wa uhusiano wa umma katika kampuni ya ubashiri ya sportpesa ambao ni wadhamini wa shati ya kogalo wamewapongeza Gor Mahia kwa kushinda ubingwa wa ligi hiyo na kuwaahidi kuwazawadi kitita cha shilingi milioni 3.5 kutokana na juhudi zao za msimu mzima.
Benson Omala, mshambuliaji wa klabu ya Gor Mahia ndiye mshindi wa kiatu cha dhahabu baada ya kumpiku Elvis Rupia fowadi wa Kenya Police kimabao.
Omala msimu huu amefunga mabao 26 huku Rupia akifunga mabao 25 na hatimaye mshambuliaji wa klabu ya Bandari Abdhalla Hassan akimaliza ligi na mabao 13.
