FAITH KIPYEGON APATA NYUMBA BAADA YA KUVUNJA REKODI

Rais wa Kenya William Samoei Ruto amempongeza mwanariadha Faith Kipyegon kwa kuandikisha rekodi ya kimataifa katika mbio za mita 1500 katika mashindano ya Florence Diamond League na baadaye kuvunga rekodi nyingine ya 5000 katika mashindano ya Paris Diamond League.

”Faith ni mkenya mwenye imani sana. Imani yake ilimfanya kushinda na kuandikisha rekodi za dunia. Nampongeza sana kwa kuiheshimisha Kenya katika ngazi za kimataifa.” Alisema Ruto.

Ruto amesema kwamba Faith Kipyegon ni shujaa wa kutiliwa mfano baada ya kuwakilisha taifa hili katika viwango vya kimataifa alipokuwa amempokea katika ikulu ya Nairobi asubuhi ya leo pamoja na wanariadha wengine akiwemo Omanyala na Mary Moraa lakini pia viongozi wengine wa riadha.

Ruto ametoa hakikisho kwa wanariadha wa taifa hili kuwa serikali yake inapania kuboresha michezo hapa nchini hata zaidi kupitia uwekezaji.

”Natoa hakikisho leo kwa wanariadha wote wa Kenya pamoja na wanamichezo wengine kuwa michezo hapa nchini Kenya tutaiboresha. Tutawekeza katika michezo hapa nchini katika njia moja ya kuheshimu wanamichezo wetu ambao wanajitolea kuipa sifa Kenya yetu” Aliongeza Ruto.

Faith Kipyegon amezawadiwa na Ruto kima cha Kshs milioni tano pamoja na nyumba yenye thamani ya shilingi milioni sita katika jiji la Nairobi.