Muungano wa wanabiashara wa bodaboda mjini Malindi kaunti ya Kilifi wanalenga kuandaa mashindano ya soka ya siku moja katika uwanja wa Alaskan mjini Malindi wikendi ijayo.
Mashindano hayo ya siku moja yatakayofanyika siku ya Jumamosi yanalenga kuhamasisha wanaboda boda kuhusiana sheria za barabarani, usalama wao pamoja na kutoa hamasa kuhusu biashara hiyo.
Akizungumza na Tama la Spoti kupitia njia ya simu John Randu ambaye ni mwenyekiti wa muungano huo mjini Malindi amesema kwamba mashindano hayo yanahusisha timu za wanabodaboda pamoja na jamii kwa jumla.
”Ni mashindano yatakayofanyika tarehe 17 mwezi huu katika uwanja wa Alaskan. Tunatarajia timu za bodaboda pamoja na timu za wanajamii ambazo zitachuana pale. Katika kufanya mashindano hayo kutakuwa na mpango wa kuhamasisha hawa jamaa wa bodaboda kuhusu umuhimu wa sheria za barabarani pamoja na usalama wao barabarani. Wajua ni vigumu sana kuwakusanya hawa mabodaboda na kuwaongelesha kama vile, sasa hata hii pia ni njia moja ya kuwahamasisha kuhusu pia hii biashara.” Alisema Randu.

