SPARKI YOUTH YAGOMEA MECHI KISA UKOSEFU WA USALAMA

Mechi kati ya klabu ya Mariakani FC na Sparki Youth jana ililazimika kusitishwa kabla ya kipindi cha pili kuanza rasmi, hii ni kutokana na klabu ya Mariakani fc kukosa kuwasilisha maafisa wa polisi mapema kabla ya mechi hiyo kuanza kama kipengele katika sheria za fkf kuwa klabu ya daraja la pili kitaifa inapoandaa mechi katika uwanja wao wa nyumbani.

Akizungumza na Tama la spoti kupitia njia ya simu mchana wa leo Abdhala Ali ambaye ni mkufunzi wa klabu ya Sparki Youth amesema kwamba walilazimika kukataa kurudi uwanjani kutamatisha kipindi cha pili kutokana na kukosa hakikisho la usalama wao kutokana na wenyeji wao kukosa kuleta maafisa wawili wa polisi.

‘’ Tuliona hawa jamaa wa Mariakani wanatuchezea, waliahidi kipindi cha kwanza kabla kitamatike wataleta maafisa wa polisi lakini mpaka kipindi cha pili chaanza hawajaleta. Sisi tukalazimika kuachana na hiyo mechi. Msimamizi wa mechi aliyaona hayo na kila mtu akaafiki tusiendelee na mechi. Manake inashangaza, Mariakani kituo hata kakiko mbali lakini vipi wenzetu wakose kuleta maafisa? Tukaichukulia kama fursa ya kupewa alama kwetu na ndio hivyo tunasubiri uamuzi wa ofisi.’’ Alisema mkufunzi Abdalla.

Hata hivyo mkufunzi huyo amekanusha tetesi kuwa vilabu vya Mombasa vinapendelewa na marefa pamoja na maafisa wanasosimamia mechi zao wanapocheza dhidi ya vilabu vya kilifi katika mechi zinazoandaliwa katika kaunti ya Mombasa.

Mkufunzi huyo amesema madai ya makocha wa vilabu vya Kilifi kuhusu maonevu ni porojo kwani hata klabu yake ya Sparki imekuwa ikifungwa na vilabu kutoka kaunti ya Kilifi.

‘’Hizo ni porojo, hata mimi tayari ni wa Mombasa na timu zote za Kilifi zanifunga. Mimi sioni hao wakufunzi wanaoleta madai hayo ni ya kweli.’’ Alisema Abdalla.

Vilabu vya Kilifi vimekuwa vikisema kwamba kuna mapendeleo kwenye uongozi wa soka la daraja wa pili ambapo maonevu yanaelekezwa kwa vilabu vya kaunti ya Kilifi.