Mwanga wa Lulu Viwanjani wiki hii unamuangazia nyota ambaye mbali na kuleta tabasabu katika taifa lake Morocco ya kaskazini mwa Afrika, wiki hii aliingia katika rekodi ya wachezaji wenye mchango mkubwa katika mashindano makubwa ya Ulaya.
Ni mchezaji ambaye amepewa sifa si haba na wakufunzi ambao washawahi kumfunza soka. Mchezaji huyu ni mchezaji wa kwanza katika historia ya klabu ya Sevilla kufunga bao katika ligi ya laliga.
Nyota wetu wa wiki wiki hii ni Yassine Bounou mchezaji wa timu ya taifa ya Morocco na klabu ya Sevilla. Tunamvulia kofia kutokana na mchango wako wiki hii katika mechi ya fainali ya mashindano ya Europa ambapo klabu yake ilikuwa inavaana na AS Roma ya mkufunzi Jose Mourinho.
Katika mechi hiyo iliyochezwa katika dimba la Puskas Arena mjini Budapest nchini Hungary alipata ufalme wa uchezaji bora maarufufu kama ‘Man of the Match’ kutokana na mchango wake mkubwa.
Katika mechi hiyo ya fainali iliyokuwa na taharuki kubwa mwanzo mpaka mwisho Bounou aliweza kuokoa mipira kadhaa kutoingia wavuni ikiwemo kuishindia Sevilla kombe la saba la Europa baada ya kuokoa penalti mara mbili baada ya dakika tisini na muda wa ziada mechi hiyo kuisha sare ya bao 1-1. Katika matuta mechi hiyo iliisha kwa Sevilla kushinda AS Roma kwa mabao 4-1.
Mlinda lango huyo si mgeni katika kuokoa mipira ya matuta kwani pia alifanya kama hivyo kwenye mashindano ya kombe la dunia mwaka jana nchini Qatar na kuitoa Uhispania katika hatua ya 16 bora.
Mchango wa Bounou katika kuisaidia Sevilla kushinda ubingwa huo wa saba umeifanya klabu hiyo ya laliga kufuzu kucheza mashindano ya klabu bingwa Ulaya msimu ujao.
Rafiki, sasa tumfahamu kwa undani kabisa mlinda lango huyo ambaye amekuwa na mafanikio makubwa katika ya Sevilla kule Uhispania.
Jina lake kamili anajulikana kama Yassine Bounou (Bono) na alizaliwa tarehe 5 mwezi Aprili mwaka 1991.
Wazazi wake wote ni raia wa Morocco lakini walimzaa Montreal nchini Canada ambako walikuwa wakifanya kazi. Hata hivyo walirejea Casablanca nchini Morocco na wazazi wake akiwa na umri wa miaka 3.
Katika makuzi yake alipenda soka sana na alianza kurindima soka la kitaa vile vijana wengi mashinani wanavyokuwa Afrika na bila shaka pale mtaani kwako rafiki hilo unaliona au hata wewe huenda ushawahi cheza soka la namna hiyo – Kule wanaliita tufe.
Sasa Bounou alipenda kucheza kama mchezaji wa nafasi za ndani ya uwanja tofauti na ukipa alionao kwa sasa.
Awali wazazi wake hawakupenda acheze mpira lakini shauku yake na kupenda soka kuliwafanya wazazi hao kumwachilia aendelee na mapenzi yake ya kandanda.
Alianza rasmi soka la ushindani akiwa na klabu ya Wyadad AC na umri wa miaka nane pekee. Kutokana na urefu wake jamaa akaona heri autumie vilivyo katika nafasi isiyokuwa na ushindani sana miongoni mwa wachezaji wenza hivyo akavalia ukipa mwaka wa 1999 na hivyo ndivyo safari ya ulinda lango ilianza ilianza.
Kimataifa amechezea vilabu vikubwa laliga ikiwemo Atletico Madrid, Girona, Zaragoza na sasa klabu ya Sevilla.
Msikilizaji Bounou ni mshindi wa Laliga mara moja akiwa na Atletico Madrid msimu wa 2013/2014, pamoja na kushinda ligi ya Europa mara mbili akiwa na Sevilla.

