Klabu ya Beach Bay kutoka eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi inakadiria hasara ya zaidi ya shilingi elfu 50,000 baada ya ofisi yao kuvamiwa na kuporwa usiku wa Jumamosi wikendi iliyopita.
Kulingana na mkufunzi mkuu wa timu hiyo Peter Mole akizungumza na Tama la Spoti asubuhi ya leo ni kwamba sare pamoja na mipira lakini pia vitu vingine vilipotea na wezi ambao mpaka kufikia sasa hawajabainika.
”Tulishangaa sana hiyo siku (Jumapili) asubuhi twataka kuanza safari tunafika ofisini tunapata imefunguliwa na kumechakurwa kila mahali. Waliiba mipira, sare (pair) mbili pamoja na vitu vingine vya thamani. Kwa kweli hilo ni pigo kwani tumepoteza zaidi ya vitu vyenye thamani ya shilingi elfu hamsini,” Alisema Peter Mole.
Mbali na changamoto ya usafiri klabu hiyo ya Beach Bay siku ya jumapili walilazimika kuazima sare kutoka kwa wapinzani wao Simba Apparel katika kaunti ya Mombasa kwenye mechi ambayo walitandikwa kichapo cha mabao 5-0.
”Tuliongea ofisi tukapiga simu kwa shirikisho tulipofika Mombasa Simba Apparel wakatuazima jezi zao kuchezea mechi kisha tukawarudishia. Kwa kweli tulikuwa tumeishiwa na motisha kwani huku tumeibiwa, uwanja wanyesha na usafiri wenyewe ulitutatiza. Ila Simba walishinda kihalali manake tulikuwa chini sana kimchezo.” Aliongeza Peter Mole.

