Kocha mkuu wa kikosi cha Kilifi kwenye michezo ya KYISA inayoendelea kaunti ya Tharaka Nithi Rio Ngumbao amesema kikosi hicho kina uwezo mkubwa wa kufanya vyema zaidi baada ya kufanikiwa kufuzu katika hatua ya robo fainali.
Akizungumza baada ya kusajili ushindi wao wa kwanza kabisa kwenye ngarambe hizo dhidi ya Wajir, Rio amewasifu wachezaji wake kwa kuhimili shinikizo na kupata ushindi huo.
Hata hivyo mkufunzi Rio amelalamikia uchezeshaji mbovu kutoka kwa waamuzi akitarajia watabadilika kadri mechi zinavyopamba moto katika kaunti hiyo ya mlima Kenya.
Kwa upande wake, Nahodha wa kikosi hicho Emmanuel Sifa amesema walicheza kwa kujiamini zaidi katika mechi yao dhidi ya Wajir. Ameongeza kwamba mabadiliko ya kimfumo ya mkufunzi wake yamechangia pakubwa katika kusajili matokeo mazuri hii leo.
Sifa aidha pia anaamini Kilifi Ina uwezo mkubwa wa kumnyakua mwanamwali huyo. Kilifi sasa wanasubiri kufahamu mpinzani watakayekutana naye robo fainali.

