Wachezaji wawili wa klabu ya Mathare United inayocheza ligi kuu nchini Kenya wamesimamishwa kutoshiriki mechi yoyote ya ligi na shirikisho la soka la FKF kutokana na madai ya upangaji wa matokeo.
Wachezaji hao ni Lennox Ogutu pamoja na Alphonce Ndonye na kulingana na waraka uliochapishwa mitandaoni na FKF, uchunguzi kuhusu madai ya kupanga kwa matokeo kwa wawili hawa unaendelea na iwapo watapatikana na hatia kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za michezo.
Kwa upande wao Mathare United imethibitisha kwamba wawili hao watasalia kupigwa marufuku, na kama klabu, Mathare United sasa inalenga kutoa taarifa zaidi kuhusu hilo baada ya uchunguzi wa ziada umetamatika.
Jana klabu hii kutoka mitaa ya mabanda ilisajili ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Vihiga Bullets na huu unakuwa ushindi wao wa pili msimu huu baada ya kucheza mechi 12 ligini.

