Wakati vilabu vya hapa nchini vinapozidi kujitayarisha kwa msimu mpya wa 2022/2023 Mkufunzi wa Nzoia Sugar FC Salim Babu anatazamia michuano mikali ya ligi pindi itakapoanza rasmi.
Nzoia sugar walipoteza 1-0 na 2-0 dhidi ya Nyota FC na Wazito FC mtawalia katika mechi za kirafiki wiki iliyopita na mkufunzi Babu anasema kwamba hajashtushwa sana na matokeo hayo, akisema kuwa anazingatia jinsi timu inavyoendelea kucheza kuliko matokeo yake.
Fundi huyo wa soka anasema ari ya kupambana kutoka kwa vijana wake ndiyo kitu anachotaka kukiona mara tu msimu mpya utakapoanza.
Msimu mpya wa ligi kuu nchini unatazamiwa kuanza mwezi ujao kati ya Novemba 12 na Novemba 20 kulingana na mawasiliano ya Wakurugenzi Wakuu wa klabu za Ligi Kuu kufuatia mkutano wao wiki jana.

