Kocha mkuu wa timu ya Shabana fc inayocheza ligi ya daraja la pili maarufu kama National Super League Sammy Okoth ameiomba serikali kuchukua hatua haraka kumaliza mgogoro wake na shirikisho la soka la kimataifa FIFA ili shughuli za soka zirudi katika hali yake ya kawaida nchini.
Mkufunzi Okoth, ambaye timu yake ilimaliza nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu ya Kitaifa msimu uliopita, anasema kutokuwa na uhakika kutokana na kufungiwa kwa muda kwa Kenya na FIFA kumeleta pigo kubwa kwa shughuli za vilabu vingi kabla ya msimu mpya, kwani haziwezi kusajili wachezaji wapya au kuandaa ratiba za mazoezi.
Licha ya hali ngumu inayoikabili soka ya Kenya, mtaalamu huyo mwenye uzoefu ana uhakika waziri mpya wa Michezo Ababu Namwamba atachukua jukumu muhimu katika kurejesha shughuli za soka nchini.
Shabana itajaribu kurejea Ligi Kuu ya FKF msimu ujao baada ya majaribio manne kufeli katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

