SOKA LA KENYA KUSUBIRIWA KWA MUDA WA ZIADA – BARRY OTIENO

Mkurugenzi mkuuu wa shirikisho la soka FKF Barry Otieno amesema kwamba huenda wapenzi wa soka la FKF hasa ‘Premier League’ ya wanaume lakini pia ya kinadada wakalazimika kusubiri kwa muda zaidi kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu.

Kamati ya mpito inayosimamia soka nchini ilikuwa imeratibu ligi za wanaume pamoja na wanadada kuanza tarehe 24 na 25 mwezi huu (Septemba) mtawalia lakini sasa ujio wa maafisa wa FKF kurejea katika ofisi zao kutalazimu msimu kusubiri kwa muda wa ziada.

Kulingana na Barry Otieno sasa maafisa hao wa FKF wanalenga kufanya kazi na kila mshikadau wa soka kuhakikisha kwamba soka linarudisha hadhi yake ya awali.

Masaibu ya soka nchini Kenya yalianza kipindi ambacho wizara ya michezo nchini ilibandua shirikisho la soka na kuchagua kamati ya mpito kusimamia mechi zilizosalia, jambo ambalo liliathiri pakubwa soka kutokana na shirikisho la soka duniani FIFA kupiga marufuku Kenya kwenye michezo ya kimataifa.