YUSUF LULE ATOA WITO KWA SERIKALI KUU KUWEKA MIKAKATI YA KUKABILIANA NA UKOSEFU WA USALAMA

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu katika kaunti ya Mombasa yakiongozwa na lile ya HURIA yametoa wito kwa serikali kuu kuweka mikakati ambayo itakabiliana na visa vya ukosefu wa usalama nchini.
Yakiongozwa na mkurugenzi mkuu wa shirika la HURIA Yusuf Lule yamesema hali hiyo inaendelea kuathiri shughuli nyingi nchini pamoja na maisha ya Wakenya.
Lule amesema ukosefu wa usalama nchini umeathiri kwa kiwango kikubwa uchumi wa nchi hali ambayo imechangia kwa gharama ya maisha kupanda.
Aidha, ameitaka serikali kuu kulipa kipaumbele suala la usalama nchini Kenya ili Wakenya waendelee kuisha kwa amani bila changamoto zozote.
Naye Grace Oloo ambaye ni afisa wa shirika la UJAMAA CENTER kaunti ya Mombasa amewahimiza wazazi hasa kina mama kuwajibikia vilivyo majukumu yao ya ulezi ili kuwalinda watoto wao dhidi ya kupotoka kimaadili kauli ambayo imeungwa mkono na naibu kamishna wa kaunti ya Mombasa Ronald Mwiwawi ambaye amethibitisha kuna watoto wenye umri mdogo ambao wanajihusisha na visa vya uhalifu na kusema mikakati imewekwa ili kuwakabili.