WITO WA KUPIGA JEKI GOFU WATOLEWA

Wadau wa mchezo wa gofu kaunti ya Kilifi sasa wanaitaka serikali ya kaunti hiyo kupitia idara ya vijana na michezo kuangazia zaidi mchezo huo.

Kulingana na mchezaji gofu ambaye ni mwanachama katika klabu ya gofu ya Malindi Raphael Diwani, gofu ni mchezo ambao endapo utaangaziwa vizuri na idara husika unaweza kuwa kitega uchumi kwa wachezaji na hata washikadau.

Diwani anaamini Kilifi ni moja kati ya sehemu ambazo zina wachezaji hodari wa gofu ambao wanaweza kuiwakilisha kaunti hiyo hata katika ngazi za kimataifa, akisisitiza umuhimu wa serikali kupiga jeki sekta hiyo.

Diwani ameelezea haya baada ya kuwa mchezaji wa kwanza kwenye historia ya klabu ya gofu ya Malindi kulenga shimo la 13 kwa mpigo mmoja tu na kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu ikizingatiwa kwamba, hakuna mchezaji yeyote aliyewahi kulenga shimo hilo kwa mpigo mmoja pekee.

Anasema alijihisi mwenye furaha tele kufuatia mafanikio hayo aliyoyapata katikati mwa juma hili.

Idara ya michezo kaunti hiyo chini ya Waziri wa michezo Daktari Ruth Dama Masha imeeleza kwamba itaangazia aina zote za michezo ili kutambua talanta tofauti zilizopo.