WENYEJI WA KAUNTI YA KILIFI WAONYWA DHIDI YA MAWAKALA MATAPELI

Wenyeji wa kaunti ya Kilifi na Pwani kwa jumla wametakiwa kuwafahamu vyema mawakala wanaowasadia kupata ajira katika mataifa ya Ughaibuni, ili kurahisisha shughuli za kupata usaidizi kila wanapokuwa katika mataifa hayo.
Wakiongozwa na mwaharakati wa shirika la kuteteta haki za kibinadam la MUHURI, Afia Swaleh amesema kumekuwa na mawakala wengi ambao ni matapeli kwani hawana vibali hitajika vya kutekeleza kazi hiyo kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na wanahabari katika eneo la Malindi, amesema hatua hiyo ndicho chanzo cha kushuhudiwa kwa visa vya wengi wa wale wanaoelekea katika mataifa hayo, kukosa usaidizi baada ya kupitia mateso kutoka kwa waajiri wao.
Kwa upande wake Daniel Ngahu ambaye ni mwanaharakati na pia mkurugenzi wa shirika la JAMII KWANZA katika eneo la Malindi, amesema kuwa ipo haja ya asasi mbalimbali za serikali kuwachunguza wale wanaodai kuwa mawakala wa kusafirisha wakenya katika mataifa hayo.