Waziri wa michezo kaunti ya kilifi DR. Ruth Dama Masha ameweka wazi mikakati ya kaunti hii kwenye suala la kuanza kukuza talanta ya watu wanaoishi na uatilifu pamoja na akina dada kwa lengo la kuwapa ajira katika serikali ya kaunti.
Akizungumza na Tama la Spoti katika hafla ya mechi ya kirafiki kati ya maafisa wa polisi na wahudumu wa boda boda dimbani Alaskan mjini malindi wikendi ilopita, Masha amesema kwamba hivi karibuni kaunti ya Kilifi itakuwa na uwanja wake pindi tu uwanja wa Water mjini kilifi utakapokuwa umekamilika.
‘’Kuna mikakati ambazo tumeianzisha ya kuinua watu wanaoishi na uatilifu katika talanta zao lakini pia kuwaboreshea maisha. Hivi majuzi tuliongea na wawakilishi wadi walete vikosi vya watu hawa ili tuone tuna weza kuwasaidia vipi kama serikali.
Vilevile tunataka kuendeleza ujenzi na uboreshwaji wa viwanja katika gatuzi hili. Tunaimani hivi karibuni mbali na viwanja vinavyokarabatiwa uwanja wa Water Kilifi utakuwa umepata hadhi inayotakikana.’’ Alisema waziri Masha.
Ikumbukwe kwamba uwanja wa Water mjini Kilifi ulianza kurekebishwa na kuboreshwa mwaka 2023 katika azma ya kutumika kama kiwanja moja wapo wa kuandaa mashindano ya kitaifa ya KYISA mwezi April mwaka huu.
Mbali na uwanja huo serikali ya kaunti ikiongozwa na gavana Mng’aro imeendeleza juhudi za kujenga viwanja katika gatuzi hili na uwanja wa hivi punde zaidi ni ule wa mchezo wa mpira wa vikapu katika manispaa ya Malindi Cleopatra uliozinduliwa rasmi mwezi Novemba mwaka jana.

