Waziri wa masuala vijana, jinsia na michezo kaunti ya Kilifi Dama Masha, ameadhi kushirikiana na mashirika ya kijamii pamoja na vijana wa kaunti ya Kilifi, ili kuunda sheria ambazo zitasaidia kuhakikisha vijana wanahusishwa katika masuala ya miradi na uongozi wa kaunti ya Kilifi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuhamasisha vijana kuhusiana na masuala ya uongozi katika shirika la SAFE COMMUNITY YOUTH INITIATIVE mjini Kilifi, waziri huyo amesema kuwa hiyo itasadia vijana kuwa na uwezo wa kutoa maoni yao katika miradi ya serikali kaunti huku kauli yake ikiungwa mkono na afisa mkuu katika idara ya Ugatuzi Zamzam Mohammed, ambaye ametaja kuwepo kwa afisi ya gavana katika kila eneo bunge la kaunti ya Kilifi, kama njia mojawapo ya kufanikisha masuala ya vijana na huduma kwa jamii.
Kwa upande wake mkurungezi mkuu wa shirika hilo la SAFE COMMUNITY YOUTH INITIATIVE, Benjamin Kahindi amesema lengo kuu la kuanzishwa kwa mradi huo ni kuhakikisha vijana wanashiriki katika vikao vya kutoa maoni ya maendeleo ya serikali ya kaunti katika jamii na kuwa ni jukumu la mashirika ya kijamii pamoja na viongozi wa vijana, kushurikiana na serikali ya kaunti ili kuafikia suala hilo.
Aidha, baadhi ya vijana wakiongozwa na Jane Nzai pamoja na Moses Munga ambaye ana uwezo maalumu wameunga mkono mradi huo pamoja na hatua ya kila eneo bunge kuwa na afisi ya gavana, wakisema itawezesha wananchi kupata hudumu za afisi hizo mashinani pamoja na taarifa kuhusiana na vikao vya wananchi kupendekeza miradi ya maendeleo kwa wakati.
VIJANA KATIKA KAUNTI YA KILIFI KUHUSISHWA KWENYE MASUALA YA MIRADI NA UONGOZI WA KAUNTI YA KILIFI

