HIMIZO LATOLEWA KWA WAZAZI KAUNTI YA KWALE KUWARUHUSU WATOTO WAO WA KIKE KUCHANJWA CHANJO YA HPV

Wenyeji wa kaunti ya Kwale wameshinikizwa kuwaruhusu watoto wao wa kike walio kati ya umri wa miaka 10 hadi 14 wanapata chanjo ya kuzuia saratani ya kizazi ya HPV.
Kulingana na waziri wa afya kaunti hiyo ya Kwale, Francis Gwama saratani imeathiri zaidi ya asilimia 40 ya wanawake hivyo kuna haja ya wakaazi wa kaunti ya Kwale hasa wanawake kujitokeza kupata chanjo hiyo kuanzia tarehe 13 -17 mwezi huu wa Februari.
Gwama amesema suala la wasichana wadogo kushiriki ngono wakiwa na umri mdogo pia linaweza kuwaweka wasichana hao kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa saratani ya kizazi.
Waziri huyo wa afya amesema gharama ya kutibu saratani ni ya juu mno ila inapogundulika mapema huweza kutibika jambo linalosababisha shinikizo zake za kutaka wakaazi wafanyiwe ukaguzi wa kiafya mapema iwezekanavyo kubaini iwapo wamepatwa na saratani hiyo ya kizazi au la.