SHIRIKISHO LA SOKA LAFUNGIA KWA MDA WACHEZAJI NA MAREFA

Shirikisho la soka nchini Uganda, FUFA limetoa adhabu ya kufungiwa kwa muda, kwa wachezaji sita na waaamuzi wawili kutokana na tuhuma za upangaji matokeo katika mechi za Soka.

Washirika waliopigwa marufuku ni pamoja na waamuzi Opio Deogracious na Nkurunziza George.

Wachezaji ni Waiswa Andrew, Kakooza Yaya Mahad wanaoichezea Gaddafi FC, mchezaji wa Kitara FC Lwesibawa Godfrey, Maganda Saleh ambaye ni mlinda lango wa timu ya Calvary FC.

Pia mlinda lango wa timu ya Northern Gateway FC Oringa Franco na Mwima Abdallah anayeichezea timu ya chuo kikuu cha Ndejje wanakamilisha orodha ya waliofungiwa.

Uamuzi huo umetolewa baada ya kamati ya uchunguzi katika kamati ya maadili na nidhamu ya FUFA kufanya kikao na kusema uamuzi wao unazingatia Ibara ya 73 ya Kanuni za Maadili na Nidhamu za FUFA.