Klabu ya Bombi FC inaendelea kuselelea kileleni mwa jedwali la ligi ya kaunti ndogo ya Malindi ikiwa na alama 16 alama sawa na Black Hunters wakitofautishwa na magoli japo viongozi wa jedwali wana mechi mbili kiporo.
Real Galana FC ambao wako na alama 13 sambamba kakuyuni City na Kathana wanashikilia nafasi ya tatu, ya nne na tano mtawalia baada ya mechi 8.
Shakahola FC ambao wamecheza mechi 6 wanaendelea kushikilia nafasi mwisho kwenye jedwali wakiwa na alama moja. Wametoka sare mechi moja na kupoteza mechi tano.
Aidha mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora zimepamba moto Samuel Koi wa Real Galana na Alex Fondo wa Jilore United wakishikilia nafasi ya kwanza na ya pili mtawalia kwa kuweka kambani magoli sita huku Amani Sulubu wa Zamaleck Junior ambaye amecheka na wavu mara 4 akifunga kwenye tatu bora.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea wikendi hii.

