Naibu Gavana wa kaunti ya Mombasa Francis Thoya amesema serikali ya kaunti hiyo imeanzisha harakati za kulifunga rasmi jaa la taka lilitoko kwenye eneo bunge la Kisauni kaunti ya Mombasa ili kuboresha mazingira.
Thoya amesema serikali ya kaunti ya Mombasa imekuwa ikiyafunga majaa ya taka ambayo yamekuwa kwenye makazi ya wenyeji ili waishi katika mazingira bora.
Kulingana na Thoya ambaye pia ni waziri wa mazingira katika kaunti hiyo majaa hayo ya taka yamekuwa yakichangia kwa uchafuzi wa mazingira.
Vilevile, amewahimiza wenyeji kuchukua jukumu la kutunza mazingira kwa kutotupa taka ovyo.
Kauli yake imeungwa mkono na mwakilishi wa wadi ya Junda Sylvester Kai ambaye ametoa himizo kwa wenyeji kushirikiana na serikali ya kaunti ya Mombasa katika kuimarisha usafi katika kaunti hiyo.
Kufikia sasa jumla ya majaa 30 ya taka yamefungwa na serikali ya kaunti ya Mombasa.
SERIKALI YA KAUNTI YA MOMBASA YAFUNGA BAADHI YA MAJAA YA TAKA

