Ni rasmi sasa mkufunzi Nero Chishenga amejiunga na klabu ya Rocky FC yenye makazi yake katika mtaa wa Thalatha Mel eneo bunge la Malindi Kaunti ya Kilifi.
Kulingana na Nero ameamua kuachana rasmi na Malindi Progressive Academy na kujiunga na klabu hiyo ya Rocky ambayo zamani alikuwa akiichezea.
Ameeleza matumaini yake kuwa anatarajia kuwa na wakati mzuri katika ligi ya mkoa msimu mpya utakapoanza kwani asilimia 70 ya viongozi wa Rocky hasa katika benchi la kiufundi ni wachezaji wa zamani wa klabu hiyo.
”Naona nitakuwa na wakati mzuri kwa sababu ukiangalia uongozi wa hapa Rocky asilimia 70 ni wachezaji wa zamani wa timu hii” Alisema Nero
Nero pia amedokeza kuwa huenda Malindi Progresive Academy inayomilikiwa na mwakilishi wadi wa mji wa Malindi kaunti ya Kilifi Rashid Odhiambo isishiriki ligi msimu huu katika ligi ya mkoa.
Hii ni kutokana na mwanasiasa huyo kutaja kuwa analenga kupumzisha timu moja baada ya kusimamia timu mbili, moja ikiwa ni Malindi United inayoshiriki ligi ya daraja la pili.
Maswali sasa yameanza kuibuka kuhusu ustahimilivu wa Rashid Odhiambo kusimamia timu zake baada ya timu nyingine ya kinadada, Malindi Progressive academy Starlets kusambaratika miaka kadhaa ilopita.

