Baadhi ya wakaazi wa wadi ya Malindi mjini kaunti ya Kilifi wameandamana kulalamikia kutokuwepo kwa haki na usawa katika zoezi la uchaguzi wa wanakamati ya fedha za basari za serikali ya kaunti kwa wanafunzi wa wadi hiyo.
Kulingana na wakaazi hao kikao cha kufanya uchaguzi wa wanakamati hao, kilifanyika kinyume cha sheria na hata kinyume cha taarifa walizopewa katika barua ya mualiko, jambo ambalo wanadai lilichangiwa na mwakilishi wa wadi hiyo Rashid Odhiambo.
Wakiongozwa na Steven Oduor, Martin Chivatsi pamoja na Avia Kavata, wameibua madai kuwa mkutano huo, ulitarajiwa kuanza saa tano na wala sio saa mbili asubuhi kama ilivyofanyika na baadhi ya wale waliochaguliwa kuwa wanakamati sio wakaazi wa wadi ya Malindi mjini.
Kwa upande wake mwakilishi wa wadi hiyo ya Malindi Mjini, Rashid Odhiambo amejitenga na madai hayo na kusema licha ya yeye kutokuwa na uwezo wa kufanya uamuzi wowote kuhusiana na zoezi hilo kisheria, amepokea taarifa kuwa shughuli hiyo ilifanyika kwa njia ya haki na usawa na wananchi walipewa fursa la kupiga kura kuwachagua wale wanaohisi kuwa wanafaa kuwawakilisha katika kamati hiyo.
MWAKILISHI WA WADI YA MALINDI MJINI RASHID ODHIAMBO ANYOOSHEWA KIDOLE CHA LAWAMA

