Vuguvugu la sauti ya wanawake eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi limetoa wito kwa mashirika, wahisani pamoja viongozi wa kisiasa, kujitokeza na kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaopaswa kujiunga na shule za upili eneo hilo.
Kwa mujibu wa kiongozi wa vuguvugu hilo Bibiana Salim, kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao walipata matokeo bora katika mtihani wa kitaifa wa KCPE mwaka uliopita wa 2022, ila huenda wakakosa kujiunga na shule za upili kutokana na hali ya ukosefu wa fedha za kuwawezesha kulipa karo.
Akizungumza na lulu Fm, Bibiana amesema itakuwa bora iwapo viongozi wengi watachukua jukumu la kuwalipia karo wanafunzi hao hadi pale watakapo maliza masomo yao ya shule ya upili na wala sio kuwalipia karo ya muhula wa kwanza pekee.
Kauli yake imeungwa mkono na mwakilishi wa wadi ya Malindi Mjini kaunti ya Kilifi, Rashid Odhiambo ambaye ametoa wito kwa wanaojiweza kifedha kufadhili masomo ya wanafunzi katika jamii ili waendeleze masomo yao.
MASHIRIKA NA WAHISANI PAMOJA NA VIONGOZI WA KISIASA WAHIMIZWA KUJITOKEZA KUTOA UFADHILI WA MASOMO MAGARINI

